- Mohamed Morowa
MGENI WETU RAMADHANI
Updated: May 13, 2018

Gharibu wetu kongoni, muini kwetu ingia
Sana tulikutamani, kutwa twakufikiria
Leo tuko furahani, kwa nderemo kurubia
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Ramadhani tufungeni, matamanio tuwate
Kanuni tufuateni, ili fadhila tupate
Isilamu pulikani, nyiradi nyingi tuvute
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Mwezi ulo na neema, mtukufu Ramadhani
Thalathini siku njema, tushindeni ibadani
Tutende matendo mema, kumridhisha Manani
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Ni mwezi wa mavunoni, mwezi uso na hasara
Quruani tusomeni, na wingi wa maghufira
Na swala tuziswalini, kwa kuitendesa ghera
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Kuna usiku mmoja, ni bora hauna shaka
Huja mwaka mara moja, Ramadhani ikifika
Ukiomba zako haja, huwa zatakabalika
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Laila tul kadiri, ndo usiku wa baraka
Wala hauna dosari, wanashuka Malaika
Mola kauweka siri, tupate kuwajibika
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Maovu mwetu moyoni, wala tusiyakubali
Yanaletwa na shetwani, saumu aibatili
Kwa jaa tuyatupeni, yanaunguza amali
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Zakula tuzipikeni, nyoyo zetu kuziridhi
Tuleni kwa wasitani, afiya kuihifadhi
Isirafu tuwateni, Qudusi tusimuudhi
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Zaka tusisahauni, kwa kiwango tutoeni
Wala tusibagueni, wenye haja kuwahini
Mayatima tuwapeni, pamwe nao masikini
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani
Wetu mweni la khatima, tunamuomba Manani
Atupe afiya njema, tuifunge Ramadhani
Na kila lililo jema, lifike kwetu miini
Karibu mgeni wetu, mtukufu Ramadhani